Wednesday , 10th May , 2023

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu amefichua siri ya mazungumzo ya Maridhiano yanayosimamiwa na Mwenyekiti wake Freeman Mbowe dhidi ya Serikali kuwa ni ahadi ya chama hicho kupewa wabunge kwenye uchaguzi ujao.

Picha ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu

Mbali na kufichua siri hiyo pia Lissu ametaja ahadi nyingine ni kuwa chama hicho kitaingia katika serikali ya kitaifa aliyoiita Nusu Mkate.

Lissu alitoa kauli hiyo juzi katika eneo la Kibaigwa Mkoa wa Dodoma, akiwa katika ziara yake ya ujenzi wa Chama na kuwataka wanachama wa chama hicho wasiwachekee viongozi wao pale wanaposhindwa kukidhi matarajio yao.

Kauli hiyo ya Lissu inatajwa kuwa ni ya kujibu hotuba ya Mwenyekiti wake Freeman Mbowe,aliyoitoa Januari Mwaka huu jijini Mwanza kuwa baadhi ya viongozi wakubwa ndani ya Chama chake,wanamtuhumu kuhongwa baada ya kushiriki katika vikao vya mchakato wa maridhiano na Serikali.

Katika Mkutano huo wa Januari 31 jijini Mwanza Mbowe alieleza kuwa walipoingia katika maridhiano moja ya misingi waliyokubaliana ni Usiri wa yale waliyokuwa wakizungumza.

“Wanachama wa Chadema wakiwamo viongozi wangu wakuu ambao nawapa haki hiyo kabisa nao wanalalalamikia Usiri na kusema Mwenyekiti kalimba asali yaani Mbowe nilambishwe asali kuusaliti umma” alisema Mbowe wakati huo akiwa katika  mkutano jijini Mwanza

Hata hivyo juzi Lissu wakati akihutubia katika mji Kibaigwa alisema Kwa sasa yanaonekana mabaango mengi  mitaani kuwa Mama (Rais),amemaliza uhasama kwa kivuli cha maridhiano, jambo aliloeleza kuwa hapingani nalo.

Aliongeza kuwa kwa sasa kuna ahadi ambazo baadhi ya vyama viliwahi kupewa huko nyuma ikiwemo ahadi ya kupatiwa wabunge lakini haikutekelezwa na kwamba hali hiyo inaweza kujirudia kwenyeuchaguzi ujao.

“Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya viongozi wanadai maridhiano katikati ya madai ya watu kuuawa na wengine kufunguliwa kesi kwa sababu za kisiasa,mimi nimepigwa risasi hakuna waliokamatwa na hatujaambiwa mpaka leo,jiulizeni waliofunguliwa kesi ya Ugaidi wameombwa msamaha. Tuache ujinga na kucheka cheka kwa ahadi ya Ubunge wa kupewa na anadi ya nusu Mkate”alisema Lissu