Friday , 6th Jan , 2023

Serikali wilayani Magu mkoani Mwanza imevuka lengo la ujenzi wa vyumba vya madarasa ambapo mahitaji ya vyumba hivyo kwa kidato cha kwanza yalikuwa 271 lakini hadi sasa wamejenga vyumba 278 huku wakiwa na ziada ya vyumba saba

Afisa elimu sekondari wa wilaya hiyo ya Magu Beatrice Balige amebainisha hayo wakati wakimkabidhi vyumba hivyo vya madarasa mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima, na kusema kwa mwaka huu wanatarajia kupokea wanafunzi 10, 823 wa kidato cha kwanza

"Halmashauri ya wilaya ya Magu ilipokea kiasi cha shilingi bilioni 3 milioni 260 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 163 na seti ya meza na viti 6520 ikiwa ni fedha kutoka serikali kuu jumla vilijengwa vyumba 163 na vilivyokuwepo 115 na kufanya kuwa vyumba 278 vinavyokidhi mahitaji ya wanfunzi watakaaojiunga na kidato cha kwanza na kuwa na ziada ya vyumba saba"

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Magu Fiderica Myovela amesema fedha walizopokea za ujenzi wa vyumba vya madarasa wamehakikisha zinafanya kazi inayohitajika

"hizi fedha tulizopokea bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa tunasimamaia vizuri tumeunda kama tu ujenzi, ya manunuzi, na mapokezi lakini pia na kamati ya ufuatiliaji kwahiyo vifaa vinaponunuliwa vinasimamiwa vizuri tunahakikisha tunapoomba fedha za kununuliwa vifaa vinanunuliwa na kukaguliwa na kuelekezwa sehemu husika"

Awali akipokea vyumba hivyo vya madarasa mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima ameshukuru kasi ya ujenzi wa madarasa kwa halmashauri ya wilaya hiyo ya magu na kutaka kasi yao iendelee hivyo hivyo ili kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanasoma

"Na nyinyi ambao mmekuwa na madarasa mengi kazi imekuwa kubwa naomba nimpongeze mkuu wa wilaya na watendaji wake lakini kama nilivyosema mambo haya hayafanyiki bila nguvu na msisistizo wa wananchi kwahiyo mimi nawaomba mliofanya mipango ndani ya halmashauri ya Magu kuanza kila tunapofanya mipango ya elimu tunafikiria mipango ya elimu ya miaka 20 ijayo"