Sunday , 13th Nov , 2022

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema katika kukabiliana na upungufu wa chakula unaoweza kujitokeza kwa baadhi ya maeneo nchini, Serikali inawataka wananchi waendelee kutumia chakula kilichopo sasa kwa uangalifu na waepuke matumizi mabaya ya chakula

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Ameyasema hayo wakati akiahirisha Mkutano wa Tisa wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jijini Dodoma. Amesema katika kukabiliana na hali ya ukame na kuchelewa kuanza kwa mvua za msimu 2022/2023, wakulima waendelee kutumia mbinu bora na walime mazao yenye kuhimili ukame.

Pia, Waziri Mkuu amesema wakulima waendeleze kilimo kinachohimili ukame na chenye ufanisi mkubwa ikiwemo matumizi ya mbolea za mboji, samadi, kilimo cha matandazo ambacho huimarisha uhifadhi wa maji na unyevunyevu kwenye udongo; kupanda mbegu za mazao ya chakula yanayokomaa kwa muda mfupi na kutumia maji vizuri kwenye skimu za umwagiliaji.

“Maafisa ugani endeleeni kushirikiana na vituo vya utafiti vilivyopo kwenye maeneo yenu kwa lengo la kupata na kusambaza teknolojia za uzalishaji wa mazao, kufuatilia kwa karibu taarifa za mara kwa mara kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini ili kuwa na wigo mpana wa kuwashauri wakulima kuhusiana na hali ya hewa na kilimo kwa wakati.”