Sunday , 6th Nov , 2022

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza uchunguzi ufanyike ili kubaini watu wawili wanaozidi kwenye idadi iliyoainishwa mwanzo kuwa ndege ilikuwa na watu 43. 

Hatua hiyo imekuja baada ya kupatikana kwa miili 19 ya waliofariki huku wengine 26 kuokolewa hivyo kufanya idadi ya watu kuwa 45.

''Mili iliyopatikana hadi sasa ni 19 jumla na waliookolewa ni 26. Jumla ya waliookolewa na miili ni 45 lakini taarifa kutoka Dar na Mwanza zinasema walikuwemo watu 43. Uchunguzi ufanyike ili kujua hao wawili wanaoongezeka kwenye idadi wametoka wapi, kama ni miongoni mwa walioenda kuokoa au kama ni watumishi wa ndege hawakuandikishwa'' -  Amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Ndege hiyo ya kampuni ya Precision Air iliyokuwa inatoka Dar es Salaam kuelekea Bukoba mkoani Kagera, imeanguka ndani ya Ziwa Victoria asubuhi hii ya leo Novemba 6, 2022.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, William Mwampaghale ndege hiyo ilianguka ndani ya Ziwa Victoria baada ya kushindwa kutua kwenye uwanja wa ndege wa Bukoba.