Tuesday , 1st Nov , 2022

Naibu Waziri wa Kilimo, Mh. Anthony Mavunde aeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali yenye lengo la kuhakikisha asilimia 60 ya korosho zote zinazozalishwa nchini zinabanguliwa ifikapo msimu wa mwaka 2025/2026. 

Korosho

Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo jijini Dar es Salaam, baada ya kushuhudia mzigo tani 7.5 wa korosho zilizobanguliwa ukisafirishwa kwenda nchini Marekani na kampuni ya Ward Holding Tanzania (WHT).

"Tumeshuhudia tukio la kihistoria, ambapo korosho iliyobanguliwa nchini Tanzania inaenda kuuzwa kwa mtumiaji wa mwisho nchini Marekani, hii ni habari njema kwa wakulima wa korosho nchini na ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Rais wetu hali inayopelekea kuongeza uhakika wa masoko ya mazao ya wakulima wetu," amesema Naibu waziri Mavunde

Bei ya korosho ghafi nchini ni kati ya 1,800 hadi 2,200 ambapo unahitaji kilo tano za korosho ghafi ili kupata kilo moja ya korosho iliyobanguliwa. Wakati huo huo, bei ya korosho iliyobanguliwa nchini Marekani ni dola za Kimarekani 40 (sawa na zaidi ya shilingi 90,000 za Kitanzania), hesabu hii inaonesha dhahiri kuwa kuuza korosho iliyobanguliwa kuna manufaa makubwa kwa wakulima wetu na Taifa kwa ujumla.