
Dkt Jabir Bakari-Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
Takwimu zinaonyesha kwamba mikoa mitano nchini inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya laini za simu zinazotumika taani (Active SIM-cards) hadi Septemba 2022 ni Dar es Salaam (laini Milioni 9,756,697), Mwanza (laini 3,700,914), Arusha (3,448,200), Mbeya (3,089,848) na Tabora (3,060,407).
Ameyasema hayo leo Oktoba 25,2022 Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema uchambuzi wa laini hizo kwa watoa huduma unaonyesha kwamba kuna ushindani mkubwa kwani hakuna mtoa huduma mwenye zaidi ya asilimia 35 ya laini ya zilizosajiliwa.
"Mwelekeo wa usajili kwa miaka mitano iliyopita unaonyesha ongezeko la asilimia nane kwa mwaka. Kuenea kwa laini miongoni mwa watu kumeongezeka kwa asilimia nne kwa mwaka. Kuenea kulikuwa asilimia 78 mwaka 2017, asilimia 81 mwaka 2018 , asilimia 88 mwaka 2020 na asilimia 91 mwaka 2021". Amesema
Aidha amesema wastani wa gharama za vifurushi vya simu zilikuwa shilingi 7.8 kwa kupiga simu ndani ya mtandao Septemba 2022, kutoka shilingi 7.7 Juni 2022. Pamoja na ongezeko hili dogo, gharama bado ni chini kulinganisha na vifurushi vya simu kwenda mitandao mingine". Amesema