Tuesday , 18th Oct , 2022

Miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa na Serikali mkoani Mwanza inaenda kufungua fursa za utalii katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali, amesema Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja.

Ujenzi wa mradi wa Daraja la JPM, Mwanza

Ametaja miradi ya kimkakati itakayosaidia kukuza utalii kuwa ni ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi, ujenzi wa reli ya kisasa SGR katika eneo la Fela, meli na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Mwanza.

“Tunaamini kanda ya ziwa itakuwa ni kitovu mahususi cha utalii nchini,”- amesema Masanja.

Waziri huyo amesema uwepo wa miradi hiyo utarahisisha usafiri kwa watalii wanaotembelea jiji hilo kutoka nchi za jirani na wakati huo huo Wizara inaendelea kupanua wigo wa utalii kupitia utalii wa mikutano na utalii wa majini.

Waziri Masanja amehamasisha wananchi hususan wa Mkoa wa Mwanza kuendelea kupanda miti ili kutunza mazingira, kutunza uwepo wa hali ya hewa nzuri na kutunza vyanzo vya maji.

“Wizara ya Maliasili na Utalii ina mkakati wa kuhakikisha kila mwananchi anapanda miti miwili, hivyo imeanzisha vitalu vya miti ambayo itagawiwa kwa wananchi,”- amesema Masanja.