Wednesday , 12th Oct , 2022

Watu watatu akiwemo mtoto wa mwezi mmoja, wakazi wa Kijiji cha Rushungi, wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, wamefariki dunia na wengine 74 kukimbizwa katika vituo vya afya baada ya kula samaki aina ya Kasa mwenye sumu.

Samaki aina ya Kasa

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kijijini humo na kuthibitishwa na mamlaka husika ya ulinzi wa afya za watu mkoani humo, zimeeleza kuwa tukio hilo limetokea Oktoba 05 mwaka huu.

Baadhi ya mashuhuda wakiwemo waliohusika na ulaji wa nyama hiyo, na kupatiwa huduma katika Hosptali ya Sokoine mjini Lindi, Abdallah Mohamedi, Hassani na Ally Mussa Said walisema walikula nyama hiyo,baada ya kununua kutoka kwa watu waliokuwa wakiuza supu.

"Sisi tulikula baada ya kununua supu ya nyama hiyo,huku wengine walikula kama kitoweo majumbani mwao," wameeleza mashuhuda hao.

Aidha mashuhuda wamesema kwamba Kasa huyo aliokotwa ufukweni akiwa tayari ameshakufa, na ndipo wananchi walipoamua kugawana huku wengine wakiipika kama supu na kuiuza.

Akithibitisha kutokea tukio hilo, Mganga Mkuu wa mkoa wa Lindi Dkt. Khery Kagya, amesema ni kweli watu watatu akiwemo mtoto wa mwezi mmoja na wiki mbili wamepoteza maisha,kwa kula samaki aina ya Kasa Ng’amba anaesadikiwa kuwa na sumu.