Friday , 22nd Feb , 2019

Leo jioni kivumbi kitawaka katika Uwanja wa Taifa, ambapo matajiri wawili wa Dar es salaam, Azam FC na Simba watakapovaana katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mchezo wa Azam FC na Simba msimu uliopita

Simba inaingia katika mchezo huo ikitoka kupata pointi tatu jijini Arusha baada ya kumchapa African Lyon huku Azam FC ikiwa imetoka sare na Coastal Union.

Katika Ligi Kuu, timu hizo zimekutana mara 20 tangu Azam FC ilipopanda ligi msimu wa 2008/09, ambapo Simba imeshinda mechi 9 na Azam ikiwa imeshinda mechi 5 huku mechi 6 zikiisha kwa sare.

Kwenye historia ya mashindano yote, Simba imekutana na Azam FC mara 33, ambapo imeibukam na ushindi katika mechi 15, Azam FC ikiibuka na ushindi katika mechi 12 na mechi 7 zikiisha kwa sare.

Kuelekea mchezo huo, viongozi wa pande zote mbili wamejigamba juu ya uwezo wa vilabu vyao ambapo kila mmoja akiahidi kuibuka na ushindi. Afisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd Maganga amesema, "mchezo utakuwa ni mgumu na ushindani, kwanza kuna 'tension' nje ya timu zenyewe. Sisi kama Azam FC tunahitaji zaidi ushindi na tunaamini katika maandalizi ambayo tumeyafanya".

Naye Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu amesema, "kila game ina 'game plan' yake na ikizingatiwa kuwa hivi sasa tuna michezo mingi kila baada ya siku mbili, tunaiheshimu Azam FC na timu zote zilizopo kwenye ligi. Lakini sisi malengo yetu ni kutetea ubingwa wetu wa Tanzania ili tuweze kushiriki michuano ya Champions League mwaka ujao".

Azam FC inashikilia nafasi ya pili ya msimamo wa ligi ikiwa na pointi 50 huku Simba ikiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi 42, ambapo ligi ikiwa inaongozwa na Yanga yenye pointi 61.

Wasikilize hapa chini.