Wednesday , 20th Jul , 2022

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameunda Kamati ya watu 12 na Sekretarieti ya watu watano kwa ajili ya kumshauri njia bora za kuleta mabadiliko ya utendaji kazi wa haki kwenye vyombo vya haki jinai nchini.

Rais Samia ametoa taarifa hiyo wakati akizungumza baada ya kumuapisha Mkuu mpya wa Majeshi nchini IGP Camilius Mongoso Wambura, Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe Simon Sirro na viongozi wengine aliowateua

"Nimeunda kamati ya watu 12 na Sekretarieti yenye watu watano, Kamati hii itaongozwa na Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman ndio Mwenyekiti na makamu wake atakuwa mstaafu Balozi Ombeni Sefue, ili kunishauri njia bora ya kuleta mabadiliko ya utendaji kazi wenye matokeo bora kwenye vyombo vyetu vya haki jinai"

Rais Samia amemshukuru IGP Mstaafu Simon Sirro kwa utendaji wake huku akisitiza kuwa mabadiliko katika dunia hii hayaepukiki

"Nianze na shukrani za dhati kwa IGP Sirro, umelitumikia Jeshi la Polisi kwa muda wote, umefanya Mungu alipokujalia, umelisogeza Jeshi la Polisi, lakini jinsi dunia inavyokwenda mabadiliko lazima"

"Nimpongeze IGP Wambura, nachotegemea kutoka kwako ni kuona mabadiliko makubwa na ufanisi ndani ya Jeshi la Polisi, usalama wa raia na mali zao unaimarika ndani ya Jeshi la Polisi"

Aidha Rais Samia amesema yapo mambo yanayolalamikiwa na wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi ikiwemo Mifumo ya Upandishwaji wa vyeo hivyo serikali inaanza kuangalia suala hilo

"Tunakwenda kuangalia mifumo ya upandishaji vyeo vya taaluma, kijeshi na vyeo vya madaraka katika taasisi hizi" 

"Tunakwenda kuangalia mahusiano na raia na taasisi nyingine yakoje, malalamiko ni mengi sana, tumesema tunafungua nchi, tumeifungua wageni wanaingia wengi, malalamiko tunayoyapata kwa wageni ni mengi"

"Vitendo vinavyofanyika barabarani na Polisi, hudhani kwamba huyu kahitimu na yale anayoyafanya ni kweli kahitimu chuo, background wanazoingilia tukipekuana huko kuna feki nyingi"