Wednesday , 13th Jul , 2022

Mganga Mkuu wa serikali Dkt. Aifello Sichwale, amesema kwamba dalili wanazoanza kuzipata wananchi hadi kutoka na damu puani ni pamoja na homa, mwili kuchoka na kushindwa kupumua.

Mganga Mkuu wa serikali Dkt. Aifello Sichwale

Kauli hiyo imetolewa hii leo Julai 13, 2022, na  Dkt. Sichwale, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast cha East Africa Radio, na kusisitiza wananchi wawe na subira kwani serikali inashughulikia tatizo hilo na kila mwenye dalili hizo awahi hospitali kwa matibabu zaidi.

"Dalili wanazozipata wananchi (wanaotokwa damu puani Lindi) ni homa kali, mwili kuchoka, kupata shida ya kupumua na kutoka damu puani, timu yetu ndiyo inafuatilia ili kujua kisababishi ni nini," amesema Dkt. Sichwale

Aidha Dkt. Sichwale ameizungumzia timu iliyotumwa Lindi, "Timu yetu ambayo tumeipeleka kule, tumeitoa idara ya magonjwa ya dharura na majanga, idara ya kinga na kitengo cha magonjwa ya mlipuko, Mkemia Mkuu wa serikali wameenda kuungana na timu ya mkoa lakini wakihusisha na idara ya mifugo, tuendelee kuwa na subira,".