Wednesday , 21st Jan , 2015

Klabu ya Yanga ya jijini Da es salaam imeliomba Shirikisho la Soka nchini TFF kuwachukulia hatua wachezaji wa Ruvu Shooting, Uongozi na wote waliosimamia mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting kutokana na vitendo viovu dhidi ya Mchezaji Amis Tambwe.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Afisa habari wa Klabu ya Yanga, Jerry Muro amesema katika mechi hiyo Tambwe alishambuliwa na kuumizwa suala ambalo wasimamizi wa mchezo huo waliliona na hawakuchukua hatua yoyote dhidi ya wachezaji wa Ruvu Shooting.

Muro amesema, TFF inatakiwa kuonesha hadharani taarifa ya msimamizi wa mchezo kabla ya mchezo wa Jumamosi watakaokutana Polisi Morogoro ili kuweza kutambua kama kweli ameielezea TFF juu ya tukio hilo ambalo ni kinyume na sheria za mpira wa miguu.

Muro amesema, Mwanasheria wa Klabu hiyo anaandaa barua kwa ajili ya kuwaelezea TFF na chama cha waamuzi nchini kuwa iwapo watawapanga waamuzi waliochezesha mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting katika mechi za aina yoyote, watagoma kucheza mechi hiyo kwani tukio hilo linaonesha wazi kuihujumu timu hiyo.

Kwa upande wake, Mchezaji Amisi Tambwe amesema, tukio lililotokea kwa upande wake sio la kimpira bali ni vita hivyo anaiomba TFF kuweza kuchukua hatua kwani wakiliacha tukio hilo yanaweza kutokea matatizo makubwa zaidi ya hayo.

Tambwe amesema, katika soka kuna teknolojia ambayo huonesha matukio mbalimbali ya mechi ambapo kama Tanzania ingekuwepo, kungekuwa na urahisi wa kuona tukio hilo na hatua kuchukuliwa kwa haraka japo tukio hilo lilionekana.