Wednesday , 14th Jan , 2015

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Titus Kamani ameiagiza mamlaka ya mji wa Tunduma na halmashauri ya wilaya ya Momba mkoani Mbeya kuanza mchakato wa ujenzi wa soko la samaki na mazao mengine ya uvuvi katika mpaka wa Tanzania na Zambia mjini Tunduma

Ghala la Samaki lililotembelewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi

Dkt. Kamani amesema lengo la soko hilo ni kuweka mazingira mazuri ya biashara ya samaki pamoja na kuwezesha serikali kukusanya ushuru wa bidhaa hiyo kirahisi.
  
Waziri wa mifugo na uvuvi, Dkt. Titus Kamani ametembelea mpaka wa Tunduma kujionea hali ya biashara ya samaki na mazao ya uvuvi kwenye mpaka huo, ambako ameshuhudia biashara hiyo ikifanyika kiholela, huku akielezwa na wenyeji wake kuwa  suala la udhibiti wa biashara hiyo ni gumu kutokana na mazingira ya mpaka huo
 
Baada ya kujionea hali ya biashara ya samaki ilivyo katika mpaka huo wa Tunduma, Dkt. Kamani akatoa agizo la kuanza mchakato wa ujenzi wa soko la samaki mjini Tunduma ili kuweka mazingira mazuri ya biashara ya samaki na mazao ya uvuvi kwenye mpaka huo.

Mkurugenzi wa halmashauri ya mamlaka ya mji wa Tunduma, Juma Kitabuge, amesema kuwa  tayari eneo la ujenzi wa soko la kisasa la  samaki limeshapatikana na halmashauri inatafuta fedha za kuanza ujenzi huo.