Mtoto aliyekuwa ameibiwa akiwa na kamanda wa Polisi pamoja na mama wa mtoto
Jeshi la polisi mkoa wa Mara kwa kushirikiana na wenzao wa nchi jirani ya Kenya wamefanikiwa kuwakamata watu wawili kwa tuhuma za kumwiba mtoto Diana Meshack mwenye umri wa miezi saba mkazi wa Makoko katika manispaa ya Musoma kisha kufichwa nchini humo huku waibaji hao wakiomba kupewa milioni tatu ili waweze kumrejesha mtoto huyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara ACP Philip Alex Kalangi, amesema kuwa mfanyakazi wa ndani Paulina Sobe alikula njama na kutoweka na mtoto huyo hadi nchini Kenya kabla baadhi ya watuhimiwa hao kuanza kumpigia simu mama mzazi wa mtoto Gaudioza Meshack wakitaka kutoa kiasi cha shilingi milioni Tatu ili waweze kumrejesha mtoto huyo.
Kamanda Kalangi amewataja watuhumiwa ambao tayari wamekamatwa wakiwa na mtoto huyo huku akisema mfanya kazi wa ndani bado anatafutwa na kwamba taratibu zimefanyika za kuleta watuhumiwa nchini kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria ambao ni Vicent Magesa na Erick Range wote wakazi Getabwaga nchini Kenya.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la matukio ya wizi wa watoto ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya watu wakiwemo wafanyakazi wa ndani na baada kufanya vitendo hivyo wamekuwa wakilazimisha kupewa fedha kama moja ya sharti la kurejesha watoto katika familia zao.