
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, wa pili kutoka kushoto, akiwa na timu yake
Mhandisi Gabriel ameeleza hayo wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi inayotekelezwa kwa fedha za serikali kuu ikiwemo mradi huo wa chanzo hicho kipya cha majisafi cha Butimba.
“Nimeridhishwa na shughuli inayoendelea hapa; ikumbukwe kwamba huu ni mradi wa kimkakati ambao Serikali imewekeza fedha nyingi ili kutatua adha ya upungufu wa upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wakazi wa Jiji la Mwanza,” alisema Mhandisi Gabriel.
Amesema anatambua uwepo wa mgawo wa huduma ya maji kutokana na hali halisi ya mahitaji ambayo ni makubwa kuliko uzalishaji wa maji wa sasa wa MWAUWASA; hata hivyo alibainisha jitihada mbalimbali za Serikali ya awamu ya sita inayooongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha huduma ya majisafi inaimarika zaidi.
“Tunamshukuru sana Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira yake ya dhati ya kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani, fedha za miradi zipo na zinafika kwa wakati na miradi inaendelezwa kwa kasi,” alisema Mhandisi Gabriel.
Akizungumzia utekelezwaji wa mradi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele alisema mradi unatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya SOGEA SATOM na VINCI GRAND PROJETS kutoka Ufaransa.
“Shughuli za usanifu na ujenzi zilianza rasmi Februari, 2021 na tunatarajia ifikapo Februari 2023 mradi utakuwa umekamilika na Chanzo hiki kitakapokamilika kitaboresha huduma ya upatikanaji wa majisafi kwa wakazi zaidi 400,000 katika jiji la Mwanza na maeneo ya pembezoni kama vile Usagara, Kisesa, Buhongwa Mashariki, Lwanhima, Sahwa, Fumagila, Kishiri, Igoma na Buswelu,” alisema Mhandisi Msenyele.