
Apronius Mbilinyi - Mchumi
Hayo yamesemwa na Apronius Mbilinyi ambaye ni Mchumi alipokuwa akielezea Mustakabali wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ndipo akagusia suala la Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini kuwepo kwa matumizi mabaya ya mali za umma ambapo amesema kuwa mara nyingi Ripoti za CAG mbali na kuonesha sehemu gani ina madudu mengi ila Mamlaka husika zimekuwa zikishindwa kuwawajibisha.
“Kuna vitu vingine kwenye Ripoti za Mkaguzi mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) havisemwi hadharani lakini ukichunguza utakuta kuna sehemu hizo pesa za umma zimekwenda kwakuwa hatuna mfumo Imara wa kuwawajibisha watumishi hao kesi huishia kuzungumzwa tu”Apronius Mbilinyi_Mchumi.
Pia amesema kuwa wananchi wamekuwa wakiishia kulalamika pale wanapoona serikali haitendi vyema badala ya kutimiza wajibu wao wa kikatiba.
“Pengine hata sisi wananchi hatutimizi wajibu wetu, kwasababu wajibu wa kila mtanzania ni kuiwajibisha Serikali pale inapokwenda tofauti na Sheria za nchi”Apronius Mbilinyi_Mchumi.
Hata hivyo amegusia mwenendo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 na kusema kuwa mpaka sasa bado kuna mahali imeshindwa kutekelezwa kwa kiasi kile hususani kwenye kupambana na umaskini ambapo bado kuna hali mbaya kwa maeneo mengi inayotokana na mfumuko wa bei.
“Dira ya Taifa inapaswa kujikita zaidi katika kuboresha maisha ya watanzania kwenye nyanja zote za kiuchumi, kisiasa na kijamii”. Apronius Mbilinyi_Mchumi.
Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 ilipitishwa kuwa muelekeo wa kupandisha uchumi wa Taifa ndani ya miaka mitano ikiwa na lengo la kupambana na umaskini, kuifanya nchi kuwa na uchumi wa kati, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kama Afya na Elimu lakini mpaka sasa bado miaka mitatu tu kufika ukomo wake.