Saturday , 9th Apr , 2022

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, alituachia somo kubwa la uzalendo wa kweli kwa taifa na kulipigania 

Rais Samia ametoa kauli hiyo wakati akishiriki Mdahalo wa Kitaifa wa kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere leo tarehe 09 Aprili, 2022 uliofanyika katika Shule ya Uongozi Kibaha, Pwani.

“Mimi binafsi naona somo kubwa alilotufundisha Mwalimu Nyerere ni uzalendo kwa taifa letu, yeye mwenyewe alikuwa mzalendo wa kweli asiyetiliwa shaka, alilipenda taifa lake na kuwa tayari kujitoa muhanga kwa ajili ya watanzania”

Aidha Rais Samia amesema umoja na mshikamano ni jambo jingine ambalo linapaswa kutizamwa katika uongozi wa Mwalimu Nyerere na kuongeza kuwa alikuwa akihimiza watanzania kuwa kitu kimoja bila kujali dini, kabila, rangi wala itikadi za watu

Rais Samia ameweka wazi kuwa katika miaka ya hivi karibuni misingi hiyo iliyumba na sasa Tanzania ina kazi ya kuirejesha Tanzania kuwa kitu kimoja
“Katikati hapo tulitetereka tukaanza kujuana kwa dini, rangi, ukabila, itikadi, na ukanda, kwa hiyo tuna kazi ya kurudi kuifanya Tanzania kuwa moja” 

Katika hatua nyingine pia Rais Samia amesema Mwalimu Nyerere alihimiza matumizi ya Kiswahili kama nyenzo ya muhimu katika maendeleo ya taifa la Tanzania