
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifello W. Sichalwe.
Kwa mwaka 2019/2020 kulikuwa na jumla ya wagonjwa 9,804,356; mwaka 2020/2021 wagonjwa 8,503,409 na mwaka 2021/2022 wagonjwa 3,316,884. Takwimu hizi ni za miezi minne (Desemba hadi Machi) kwa miaka husika.
Aidha, ufuatiliaji wa mafua makali (Influenza) naofanywa katika mikoa 14 kwenye hospitali 18 nchini umebaini uwepo wa kirusi cha Influenza ambapo kati ya sampuli 1,843 zilizopimwa kwa kipindi cha tarehe 12 Desemba 2021 hadi 13 Machi 2022, jumla ya sampuli 55 (3%) zilionekana kuwa na virusi vya Influenza A inavyosababisha mafua makali na Nimonia.
Kirusi hiki kimekuwepo hapa nchini kwa muda mrefu na siyo kirusi kipya. Kwa ujumla, kiwango cha maambukizi ya kirusi hiki kinaonesha kupungua ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo kilikuwa cha wastani wa 5% hadi 6%.
Mnamo tarehe 22 hadi 25 Machi 2022 Wizara ilituma timu ya wataalam kwenye Mkoa wa Dar es Salaam kupita katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kufuatilia magonjwa haya ya mfumo wa njia ya hewa kwa watoto waliokuwa wamelazwa wenye umri chini ya miaka 12.
Takwimu zilizokusanywa zinaonesha ongezeko la wagonjwa wenye dalili za homa, kukohoa, mafua, kubanwa kifua na maumivu ya mwili tangu mwezi Desemba 2021 hadi tarehe 25 Machi 2022, ingawa takwimu hizo zilionesha kupungua kulinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita.
Taarifa hii imetolewa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifello W. Sichalwe.