Tuesday , 23rd Dec , 2014

Waziri mkuu wa zamani Mh Edward Lowassa amesema matokeo mabaya ya mtihani wa darasa la saba katika shule za msingi zilizoko maeneo ya wafugaji ni janga na pia ni kikwazo kukubwa cha jitihada za kukabiliana na Umasikini.

Waziri mkuu wa zamani Mh Edward Lowassa.

Kufuatia hali hiyo Mh Lowasa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli amewataka viongozi wakiwemo Madiwani, walimu na wazazi kukutana pamoja na kutafuta sababu za wanafunzi kufanya vibaya ili hatua za haraka zichukuliwe kwa waliochangia hali hiyo .

Akizungumza na wananchi wa kata ya Lokisale Mh Lowasa amesema pamoja na kuwepo kwa baadhi ya changamoto inasikitisha kuona hata kwenye shule zenye walimu wa kutosha , miundombinu bora na watoto wanapata chakula shuleni zimefanya vibaya utaratibu ambao amesema haukubaliki na haipaswi kuendelea kuwepo.

Wakizungumzia changamoto hiyo baadhi ya wazazi pamoja na kukiri kuwa watoto walikuwa wanapata chakula shuleni wamesema zipo changamoto nyingine nyingi ikiwemo ya usimamizi na ufuatiliaji wa huduma zinazotolewa.

Nao baadhi ya wazee wa mila wamesema tatizo la wanafunzi wengi kukaa mbali na shule pia linachangia kwani asilimia kubwa ya wanafunzi licha ya kuchelewa kufika na kupitwa na vipindi wengine wanashindwa kwenda kabisa hasa wakati wa mvua jambo linalosababisha wapitwe na vipindi vingi vya masomo.

Katika mkoa wa Arusha wanafunzi wa shule zote za wafugaji hawajafanya vizuri kwenye mitihani ya darasa la Saba na Ngorongoro imekuwa wilaya ya mwisho ikifuatiwa na Monduli na Longido