Friday , 12th Dec , 2014

Madereva watatu wa mabasi ya abiria yanayofanya safari zake kati ya Mbeya na Dar es salaam wanashikiliwa na polisi Mkoani Mbeya, baada ya kukutwa wakijiandaa kusafirisha abiria wakiwa wamelewa,

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Butusyo Mwambelo.

Aidha mabasi mengine matatu pia yakitozwa faini na mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa majini na nchi kavu, sumatra kwa kosa la kutokuwa na madereva wawili pamoja na vibali vya kusafirisha abiria.

Jeshi la polisi kupitia kikosi cha usalama barabarani kwa kushirikiana na mamlaka ya usafiri wa nchi kavu na majini nchini SUMATRA jana alfajiri wamefanya ukaguzi wa kushtukiza katika kituo kikuu cha mabasi Jijini Mbeya na kuwabaini madereva hao watatu wakiwa wameshikilia usukani wa mabasi tayari kwa kusafirisha abiria huku wakiwa wamelewa.

Baada ya kuwatia mbaroni madereva hao, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Butusyo Mwambelo ametoa wito kwa wamiliki wa mabasi kutoajiri madereva walevi huku pia akiwaonya madereva kujiepusha na ulevi wakati wakiendesha magari.

Kwa upande wake Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafirishaji wa nchi kavu na majini SUMATRA, Denis David amesema katika ukaguzi wake amebaini mabasi matatu yanayosafiri umbali mrefu yakiwa na dereva mmoja badala ya madereva wawili pamoja na basi moja ambalo halikuwa na leseni wala kibali cha kusafirisha abiria mkoani Mbeya.