
Romelu Lukaku akipiga mpira kufunga penalti kwenye mchezo dhidi ya Lazio kwenye mchezo wa ligi kuu ya Italia 'Serie A'.
6 – Ni idadi ya michezo aliyocheza mshambuliaji Yusufu Mhilu mwenye umri wa miaka 24 alipokuwa na klabu ya Yanga kwenye michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika msimu wa mwaka 2018 kabla ya kuhamia kwenye klabu ya Kagera Sukari ambapo alicheza kwa misimu miwili na kufanikiwa kufunga mabao 16 ya michezo Ligi peke ake na kuwa mchezaji tegemeo.
Kiwango hiko kimewafanya Mabingwa wa VPL wa msimu ulioisha wa mwaka 2020-2021, Wekundu wa Msimbazi Simba kumsajili na kumthibitisha usiku wa jana kupitia akaunti zao za mitandao ya kijamii huku ikiaminika nyota huyo amesaini kandarasi ya miaka miwili kuwatumikia Mabingwa hao hadi mwishoni mwa msimu wa mwaka 2023.
5 – Ni idadi ya magoli aliyofunga Samantha Kerr mshambuliaji wa timu ya taifa ya Australia mwenye miaka 25 kwenye michuano ya Olympic kwa upande wa soka la wanawake na kushika nafasi ya nne kwa wakali wa kufumania nyavu kinara akiwa Viviane Meidema wa timu ya taifa ya Uholanzi mwenye mabao 10.
Samantha Kerr anatazamiwa kuiongoza timu yake ya Australia kucheza dhidi ya timu ya taifa ya Marekani kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya mshindi watatu wa michuano ya Olympic kwa upande wa soka la wanawake,mchezo utakaochezwa saaa 5:00 Asubuhi ya leo kwenye uwanja wa Kashima na mshindi wa mchezo huo akitaraji kuambulia medali ya shaba.
Mchezo wa fainali utawakutanisha timu ya taifa ya wanawake ya Sweden dhidi ya Canada mchezo unaotaraji kuchezwa siku ya kesho Agosti 6 saa 11:00 jioni kwenye uwanja wa New Nation jijini Tokyo nchini Japan kuwania medali ya dhahabu.
4 – Ni idadi ya siku zilizopita tokea michuano ya CECAFA KAGAME CUP ianze kutimua vumbi Agosti Mosi mwaka huu kwenye viwanja vya Benjamin Mkapa na Chamazi vilivyopo jijini Dar es Salaam huku michezo sita ya hatua ya makundi ikiwa imeshachezwa na kushuhudia Yanga ikitoka suluhu na Atlabara ya Sudan kusini huku Express 1-1 Nyasi BB usiku wa jana.
Michuano hiyo inatazamiwa kuendelea tena siku ya leo Alhamisi ya Agosti 5 kwa michezo miwili, KMKM kutoka visiwani Zanzibar watamenyana na mabingwa watetezi wa micguano hiyo timu ya KCCA ya Uganda saa 10:00 jioni ilhali Azam watakipiga na timu ya Messager Ngozi ya Burundi saa 1:00 usiku kwenye dimba la Chamazi.
3 – Ni idadi ya medali za ushindi alizovaa kocha Pitso Mosimane mwenye miaka 57 raia wa Sfrika Kusini baada ya kufanikiwa kutwa kombe la michuano ya klabu bingwa Afrika mara tatu na kuwa kocha pekee barani Afrika kufanya hivyo. Mosimane alitwaa kombe hilo mwaka 2016 akiwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika kusini na mara mbili na Al Ahly ya Misri, 2020&2021.
Kocha huyo ambaye ni wa kwanza kutoka kusini mwa Afrika Kuifundisha timu ya Al Ahly anataraji kukiongoza kikosi chake kukipiga dhidi ya Mabingwa wa kombe la Shirikisho, klabu ya Raja Cassablanca kwenye fainali ya CAF SUPER CUP Septemba mwaka huu kwenye uwanja wa Jassim Bin Hamad uliopo Doha nchini Qatar baada CAF kuipanga tarehe hiyo usiku wa jana.
2 - Ni idadi ya rebound alizopiga mcheza kikapu nyota wa timu ya taifa ya Marekani, Kevi Durrant kwenye mchezo uliopita wa robo fainali ya michuano ya Olympic na kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa alama 95-81 dhidi ya timu ya taifa ya Hispania na Marekani kutinga hatua ya nusu fainali ambayo watacheza dhidi ya Australia dakika mbili zijazo .
Mchezo wa nusu fainali ya pili ya mchezo huo wa mpira wa kikapu utaikutanisha timu ya taifa ya Ufaransa ambao watachuana vikali na Slovenia saa 8:00 mchana wa leo kwenye uwanja wa Saitama Super Arena uliopo Tokyo nchini Japan.
1 - Ni idadi ya goli alilofunga mshambuliaji Romelu Lukaku alipokuwa anaichezea timu yake ya taifa ya Ubeligiji ya vijana chini ya umri wa miaka 18 mwaka 2011.
Lukaku mwenye umri wa miaka 28 ambaye kwasasa anakipiga katika klabu ya Inter Milan ya Italia, inaelezwa ameiambia klabu yake ifikirie na kukubali ofa ya klabu ya Chelsea ya paundi milioni 100 za England sawa na zaidi ya bilioni 300 za kitanzania na uwezekano wa kumuongeza mlinzi wa kushoto Marcos Alonso kama sehemu ya dili hilo ili atimkie Kwenye klabu yake ya zamani aliyoichezea michezo 15 mnamo mwaka 2011-2014 na kuhamia Everton akiwa na miaka 21.
Lukaku kwasasa amekuwa miongoni mwa washambuliaji lulu sokoni baada ya kuonesha uwezo mkubwa wa kupachika mabao, mabao 24 na assist 11 na kuisaidia Inter Milan kuchukua ubingwa wa Serie A msimu uliopita ikiwa ni kwa mara ya kwanza baada ya miaka kumi wakiwa na kocha Antonio Conte.