Wednesday , 4th Aug , 2021

Jeshi la Polisi mkoani Kagera limesema linawashikilia viongozi sita wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko uliolenga kuhatarisha amani.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi, amesema kuwa walipata taarifa la kufanyika kwa mkutano huo katika eneo la Kashai lililopo katika Manispaa ya Bukoba leo Agosti 04 mwaka huu, na kwenda kuwakamata viongozi hao sita ambao majina yao yamehifadhiwa kutokana na uchunguzi kuendelea.

“Leo majira ya asubuhi tulipata taarifa kuna maandalizi yakufanyika mkutano huo na kikao hiko chenye lengo la kushinikiza wafuasi wao na wananchi wengine washiriki kwenye shughuli hii, ambayo tayari kwenye jicho la sheria ni batili kwa sababu wanachokishinikiza ni kesi ambayo tayari ipo mahakamani na tayari viongozi wa ngazi ya kitaifa wameshaitolea maelekezo kwamaba jambo ambalo lipo mahakamni si ruhusa kulijadili nje ya Mahakama,” amesema Kamanda Malimi.

Kamanda Malimi ameeleza kuwa wamewakamata viongozi hao wakiwa tayari katika eneo la tukio na walikuwa na vifaa kwa ajili ya kufanikisha zoezi lao ikiwemo mabango ambapo jeshi la polisi limeona kama ni uchochezi.

Aidha, Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa wananchi ambao licha ya ufafanuzi uliotolewa bado wanakusudia kufanya vitendo vya uchochezi wa kuvuruga amani mkoani humo huku wakiomba viongozi wa siasa kufanya shughuli zao bila kuvuruga amani.