Tuesday , 3rd Aug , 2021

Nyota wa timu ya Phoenix Suns, Chris Paul yu mbioni kusaini kandarasi mpya ya miaka minne itakayo mfanya mkali huyo wa assist kusalia na Suns hadi mwaka 2025 ambapo atakuwa anatimiza umri wa miaka 40.

Chris Paul akijaribu kuutupia mpira kwenye kikapu na kumuacha Khris Middleton wa Milwaukee Bucks akiwa hana cha kufanya kwenye moja ya mchezo wa fainali ya NBA msimu huu.

Paul ambaye alikuwa sehemu kubwa ya kuisaidia Suns kufika fainali ya NBA kwa mara ya kwanza baada ya miaka thelathini, inaelezwa atasaini kandarasi hiyo mwishoni mwa juma hili baada ya mkataba wake kutazamiwa kumalizika Agosti 6, 2021 siku ya Ijumaa ambapo atakuwa huru.

Mkataba wake unaelezwa kuwa na tahamni ya dola milioni mia moja ishirini za kimarekani ambayo ni sawa na bilioni 278 na zaidi ya milioni 268 za kitanzania na kusaini mkataba pamoja na mlinzi pacha, Cameron Payne atakayesaini kandarasi ya miaka mitatu kwa dola za kimarekani milioni 19.

Thamani ya kandarasi ya Cameron Payne ni sawa na bilioni 44 na zaidi ya milioni 59 za kitanzania.

Kitendo cha Paul kukaribia kumwaga wino kilitabiriwa baada ya nyota huyo kunena maneno yaliyoashiria kuwa yu tayari kuendelea kusalia Suns baada ya mchezo wa mwisho wa fainali ya NBA waliyopoteza dhidi ya Milwaukee Bucks kwa series 4-2.

Paul alisema: “Huwa najifikiria mimi na kuangalia ni namna gani naweza kufanya na kujiongezea ubora, kipi nifanye zaidi na kuhakikisha narudi msimu ujao na kukifanya tena vizuri zaidi”.