Wednesday , 28th Jul , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshiriki katika makabidhiano ya miradi mipya ya iliyofanywa na nchi ya Ujerumani katika Hospitali ya Lugalo ambapo amelipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kazi nzuri ya kulinda mipaka ya nchi.

Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata Utepe kwa ajili ya kupokea Miradi iliyofadhiliwa na kujengwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Jeshi la Nchi hiyo (GAFTAG) kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ, Lugalo Jijini Dar es salaam.

Rais Samia ametoa pongezi hizo baada ya kuweka jiwe la msingi katika Kituo cha Kijeshi cha Magonjwa ambukizi kilichopo hospitalini hapo na kulitaka JWTZ kuhakikisha wanalinda miundombinu ya miradi hiyo iliweze kudumu kwa vizazi na vizazi.

“Nitumie fursa hii kulipongeza JWTZ kwa kazi nzuri ya kulinda mipaka yetu kwa hakika mnafanya kazi kubwa, kwa kutuwakilisha vyema kwenye mission za kitaifa hususan DRC na Afrika za Kati, serikali itaendeleza jitihada za kuimarisha jeshi letu ikiwemo kupata zana za kisasa na kuangalia maslahi yenu,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amegusia upandishwaji madaraja kwa wanajeshi ambapo amesema, “Nilikuwa na ugomvi na CDF juzi, aliniletea batch la mwanzo lakupandisha vyeo nikalipitisha juzi akaniletea lingine nikamuuliza vipi sinilishapandisha akajitetea sana, ntakwenda kuangalia kwa sababu najua ni sehemu ya maslahi yenu endeleeni kuchapa kazi kwa bidii,” amesema Rais Samia.

Akizungumza kuhusu kituo kilichowekewa jiwe la msingi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo amesema kituo hicho kimegharimu shiling bilioni 10.5 kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika ambao ni ufungaji wa vifaa vya kisasa na kuifanya idara hiyo kuwa miongoni mwa wa idara ya kitaifa za kudhibiti magonjwa ya kuambukiza.