Wednesday , 7th Jul , 2021

Timu ya Phoenix Suns imeanza vizuri kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza wa fainali ya Ligi ya kikapu nchini Marekani 'NBA' baada ya kuinyuka timu ya Milwaukee Bucks kwa alama 118-105 kwenye dimba la Phoenix Suns Arena saa 10:00 Alfajiri ya kuamkia leo.

Nyota wa Suns, Chris Paul akiurusha mpira kwenye kikapu baada kuwapita walinzi wa Milwaukee Bucks kwenye mchezo wa kwanza wa fainali ya NBA Alfajiri ya kuamkia leo ambapo Suns walishinda kwa alama 118-105.

Ushindi huo umechagizwa na muendelezo wa kiwango bora cha nyota wa Suns, Chris Paul aliyeibuka kuwa nyota wa mchezo baada ya kufikisha alama 32, rebaundi 4 na assit 9 na kumpiku nyota tegemezi wa Bucks wa sasa, Khris Middleton aliyeambulia alama 29, rebaund 7 na assist 4.

Nyota mwengine anayetazamiwa huenda akawapiku Chris Paul na Khris Middleton na kuwa mchezaji bora wa fainali hizo 'MVP', Devin Booker wa Suns ameondoka na alama 27, rebaundi 2 na assist 6 na kumfanya kushika nafasi ya tatu kwa wachezaji waliongáa kwenye mchezo huo.

Mchezo huo uliosheheni wachezaji nyota wenye viwango bora kwa msimu huu ulikuwa wa kukata na shoka hadi kushuhudia Deandre Ayon akipata alama 22, rebaundi 19 ilhali Giannis Antetokounmpo aliyerejea dimbani baada ya kuwa nje wiki iliyopita akionesha kiwango bora.

Giannis ambaye pia hakuwa na uhakika kucheza mchezo huo kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti alifikisha alama 20, rebaundi 17 na assist 4 huku Jrue Holiday wa Bucks akiambulia alama 10, rebaundi 7 na assist 9 hivyo kufanya ushindani wa MVP kuwa mkubwa sana.

Wachezaji 6 wanaotazamiwa huenda mmoja wao akatwaa tuzo ya 'MVP' wa fainali hizo za NBA ni watatu kutoka Phoenix Suns, Chris Paul, Devin Booker na Deandre Ayton na watatu kutoka Milwaukee Bucks, Giannis Antetokounmpo, Khris Middleton na Jrue Holiday.

Wawili hao wanataraji kushuka tena dimbani usiku wa saa 9:00 wa kuamkia tarehe 12 Julai 2021 kwenye mchezo wa mzunguko wa pili ambao pia utapigwa kwenye dimba la Phoenix Suns Arena.