Wednesday , 13th Jul , 2016

Wapinzani wa Yanga SC katika mchezo wa mwisho mzunguko wa kwanza Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika kati ya wenyeji, Medeama FC ya Ghana wanatarajiwa kuwasili hapo kesho.

Yanga watakuwa wenyeji wa Medeama FC ya Ghana Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa tatu wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Marefa wa Misri Ibrahim Nour El Din atakayepuliza filimbi akisaidiwa na Ayman Degaish na Samir Gamal Saad ndiyo watakaochezesha mchezo huo, wakati Kamisaa atakuwa Pasipononga Liwewe wa Zambia na maofisa wasimamizi ni Mfubusa Bernard ambaye atasimamia utendaji wa waamuzi wakati Mratibu Mkuu wa mchezo huo kutoka CAF atakuwa Ian Peter Keith Mc Leod.

Yanga SC itashuka kucheza na Medeama huku ikimkosa beki Mwinyi Hajji Mngwali, viungo Deus Kaseke na Geoffrey Mwashiuya katika mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi.

Kwa upande mwingine Yanga bado inaendelea kuangalia hali za wachezaji wengine ambao wanaendelea na mazoezi mepesi akiwemo mshambuliaji wa kimataifa AmisTambwe, Matheo Antony, Oscar Joshua na Malimi Busungu..

Yanga inahitaji ushindi dhidi ya Medeama baada ya kupoteza mechi zote mbili za mwanzo wakifungwa 1-0 mara zote na Mo Bejaia nchini Algeria Juni 19 na TP Mazembe ya DRC Dar es Salaam Juni 28.

Yanga inayoshika nafasi ya mwisho katika kundi A itashuka kupambana na Medeama Julai 16 mwaka huu Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam ambapo itatakiwa kushinda mchezo huo ili kufufua matumaini ya kusonga mbele katika michuano hiyo.