Wednesday , 30th Jun , 2021

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amekutana na mwenyekiti wa kundi la maseneta wa kifaransa marafiki wa Tanzania Mhe. Ronan Dantec ambapo amemuomba kuendelea kuimarisha uhusiano zaidi na Tanzania ikiwemo kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya sita.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango (kulia) akisalimiana na mwenyekiti wa kundi la maseneta wa kifaransa marafiki wa Tanzania Mhe. Ronan Dantec (Kushoto) , leo, Juni 30, 2021, nchini Ufaransa.

Dkt. Mpango amefanya mazungumzo na Seneta Dantec, leo Juni 30, 2021, katika jengo la Bunge la Seneti Paris, kwenye mazungumzo hayo, alieleza jitihada na mafanikio ya Serikali ikiwa ni pamoja na Tanzania kufikia uchumi wa kati na utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Seneta Dantec amezungumza juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira lengo likiwa ni  kupunguza hewa ukaa duniani, nakushauri uwepo wa mfuko wa fidia kwa wale watakaothirika na masuala ya kuhifadhi na kulinda mazingira. 

Kwa upande wake Dkt. Mpango alieleza kufurahishwa na uhifadhi wa mazingira unavyofanyika nchini Ufaransa ikiwemo mji wa  Paris licha ya ukongwe wa mji huo, huku akihakikisha kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Ufaransa katika uhifadhi wa mazingira, na kuwakaribisha katika kutekeleza hilo kwa pamoja.

Pia Makamu wa Rais amesema Tanzania inazingatia uhifadhi wa mazingira lakini kwa  kulinda haki za wananchi wakati wa utekelezaji wa uhifadhi huo.

Dkt. Mpango yupo nchini Ufaransa kuhudhuria Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa (Generation Equality Forum) linalofanyika Juni 30 hadi Julai 2 ,2021 lenye lengo la kuchagiza haki za usawa wa kijinsia kama zilivyokubaliwa katika mkutano wa Beijing wa mwaka 1995, akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.