Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia Prof Makame Mbarawa
Vyombo vya habari na makampuni ya simu nchini vimetakiwa kuelimisha wananchi ipasavyo juu ya sheria na taratibu za uchaguzi wakati huu nchi inapoelekea kwenye uchaguzi mkuu hapo mwakani huku Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA ikitakiwa kutoa mwongozo kwa makampuni ya simu.
Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia Prof Makame Mbarawa ametoa wito huo jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua mkutano wa kimataifa wa umoja wa mawasiliano Afrika ambapo amesema mchakato wa kutoka kwenye analojia kuingia dijitali haikuwa kazi rahisi kwani baadhi ya wadau walipinga mfumo huo kwa madai kuwa ni mapema huku akimpongeza mwenyekiti wa MOAT Dk Reginald Mengi kwa ushirikiano alioutoa kipindi chote hicho.
Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya mawasiliano Tanzania TCRA Prof John Nkoma akizungumza katika mkutano huo amesema mkongo wa taifa uliougharimu serikali dola za kimarekani milioni 200 bado haujatumika ipasavyo katika sekta ya utangazaji na kuongeza kuwa mkongo huo pia unategemewa na nchi za Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia na Malawi.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na mwenyekiti wa bodi ya TCRA Bw Salimin Senga ambaye amesema Tanzania ni kubwa, hivyo sekta ya mawasiliano inakabiliwa na changamoto ya namna ya kufika kila kona ya nchi na kwamba mipango ni hatua moja lakini tatizo liko kwenye utekelezaji.