Friday , 28th May , 2021

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU CP Salum Hamduni, kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma zinazowakabili baadhi ya watumishi wa Wizara ya Fedha waliosimamishwa kazi na Waziri Mkuu ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Hatua hiyo imekuja mara baada ya kuwasimamisha kazi Mkaguzi Mkuu, Mkaguzi Msaidizi pamoja na baadhi ya watendaji wa wizara ya hiyo ambapo wanadaiwa katika kipindi cha kuanzia Machi mwaka huu na kwa nyakati tofauti walijilipa mamilioni ya fedha kinyume na utaratibu na kueleza kuwa mara baada ya uchunguzi wa TAKUKURU ikithibitika kwamba tuhuma si za kweli wahusika watarejeshwa kazini.

Waziri Mkuu Majaliwa alizitaja baadhi ya tuhuma hizo kuwa ni malipo yaliyofanyika Machi 31, mwaka huu kupitia vocha 30 ya shilingi milioni 251 yakielezwa kuwa ni malipo maalum bila kutaja kazi hiyo na nani aliifanya, ambapo siku hiyo hiyo pia zililipwa shilingi milioni 198.8 kwa madai kuwa ni posho ya honoraria.

Aidha, Waziri Mkuu ameongeza kuwa Mei Mosi mwaka huu pia zililipwa shilingi milioni 184.1 na mchana wake zililipwa shilingi milioni 264 zikiwa ni malipo ya kazi maalum na ndipo Waziri Mkuu alihoji kuwa hiyo siku serikali yote ilikuwa Mwanza kwa ajili ya kusherehekea Siku ya Wafanyakazi Duniani halafu wao wakawa wanalipana posho.