Sunday , 23rd May , 2021

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limewataka wahitimu wa kidato cha sita mwaka 2021 kuhudhuria mafunzo kwa mujibu wa sheria katika kambi walizopangiwa  kuanzia Juni Mosi hadi 10, 2021 na kuwataka kufika hapo wakiwa na mahitaji muhimu kama vile nguo na nauli za kufika na kurudi majumbani.

Picha ya mtandao ikiwaonesha vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Kaimu Mkuu wa Utawala wa JKT,  Kanali Hassan Mabena amewataka vijana hao pia kuwa na nguo za kuzuia baridi, trakisuti ya kijani au bluu na nauli ya kwenda kambini na kurudi nyumbani kwao.

"JKT linawataka vijana wote kuripoti wakiwa na vifaa mbalimbali ikiwemo bukta za dark bluu, fulana ya kijani, raba za michezo rangi ya kijani au bluu, shuka mbili za kulalia rangi ya bluu bahari na soksi ndefu nyeusi,” amesema Kanali Mabena.

Kanali Mabena amezitaja kambi hizo kuwa ni Rwamkoma Mara, Msange Tabora, Ruvu Pwani, Mpwapwa, Makutupora Dodoma, Mafinga Iringa, Mlale, Itaka Songwe, Luwa, Milundikwa Rukwa, Nachingwea Lindi na Kibiti Pwani. Kambi nyingine ni Makuyuni Arusha, Oljoro JKT Arusha, Mgambo, Maramba Tanga, Bulombora  na Mtabila Kigoma.

Kanali Mabena amesema wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho waripoti katika kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuwahudumia.