Tuesday , 11th Mar , 2014

Ubinafsi na mvutano wa kisiasa vimetajwa kuwa moja ya sababu za kuzorota kwa maendeleo katika kata ya Buguruni jijini Dar es salaam nchini Tanzania.

Kumekuwa na kutokuelewana kutokana na utashi wa vyama baina ya diwani wa kata hiyo Fetanatus Magina kutoka chama tawala CCM na mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Marapa Sheikh Shughuli wa CUF juu ya mchakato wa kuibadilisha shule ya Msingi Buguruni Moto mpya na kuwa shule ya sekondari kutokana na kata hiyo kukosa shule ya msingi.

Akizungumza na East Africa Radio, mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Bururuni Mrapa amedai kuwa diwani wa kata hiyo amekuwa akitumia madaraka yake vibaya kwa kujiamualia masuala mbalimbali kinyume na makubaliano ya vikao wanavyokaa ikiwemo kufanya mkutano wa hadhara na wananchi kujadili suala la shule huku walikubaliana kutokufanya hivyo.

East Africa Radio imemtafuta diwani wa kata hiyo Bw Magina na kuzungumza naye na kudai kuwa Shekhe Shughuli amekuwa akiwashawishi wananchi kugomea masuala mbalimbali ya maendeleo katika kata hiyo na kuwa amekuwa akikataa kwenda kwenye mikutano ya hadhara.

Aidha Magina amesema kuwa anashangazwa na kauli ya Shehe Shughuli kuhusu shule kwani inaonekana hawaonei huruma watoto na wazazi wa Buguruni ambao wanasomba mbali na majumbani kwao.