Monday , 1st Feb , 2021

Abissay Stephen Jr

Tarehe 22 Januari 2021, Afisa mtendaji mkuu wa klabu ya Simba, Barbara Gonzalez alitangaza kuwa uongozi wa klabu hiyo umeandaa mashindano maalum yaitwayo 'Simba Super Cup' kwa lengo la  maandalizi kuelekea michezo ya makundi ya michuano ya klabu bingwa barani Africa.

Wachezaji wa Simba SC wakishangilia ubingwa wa Simba Super Cup 2021.

Maandalizi hayo ni kuwapa wachezaji utimamu wa mwili na kuwaweka tayari kwa michuano hiyo mikubwa Afrika ukizingatia wachezaji walikuwa mapumzikoni na baadhi yao walikuwa na timu ya taifa kwenye michuano ya CHAN inayoendelea nchini Cameroon.

Afisa msemaji wa Simba, Haji Manara akaongeza kwa kusema, ni fursa kwa wanasimba kuwaona wachezaji wapya, kocha mpya na kumpa fursa kocha mpya Didier Gomez Da Rosa kukiandaa kikosi chake hicho kipya na kuwajua wachezaji angalau kwa muda huo huo mchache uliopo.

Vilabu vya Al Hilal kutoka nchini Sudan na TP Mazembe ndiyo vilabu vilikuwa vilabu waalikwa, kucheza mashindano hayo ya Simba Super Cup ambayo pia yatawapa fursa sawa kujiweka fiti ukizingatia Mazembe na Al Hilal wapo kundi moja, kundi B katika michuano ya  klabu bingwa Afrika.

Michuano hiyo ilitimua vumbi tarehe 27 Januari 2021, siku ya Alhamis kwa mchezo mmoja, wenyeji Simba walikipiga na Al Hilal na kupata ushindi wa mabao 4-1 na kushuhudia kiwango kizuri na baadhi ya matukio ya kusisimua kutoka kwa Bernard Morisson licha ya Larry Bwalya kuwa nyota wa mchezo.

Mchezo wa pili ulichezwa tarehe 29 Januri 2021, siku ya Ijumaa ambapo Al Hilal alijitupa dimbani tena kwa kucheza na TP Mazembe na Al Hilal kuondoka na ushindi wa mabao 2-1. 

Mchezo wa kuamua bingwa ulichezwa tarehe 31 Januari 2021, siku ya Jumapili, Simba akatoa sare ya 0-0 na TP Mazembe.

Kwa mfumo wa ligi uliokuwa unatumika, Simba akaibuka kuwa bingwa baada ya kupata alama 4, baada ya kuifunga Al Hilal 2-1 na sare ya bila kufungana na TP Mazembe. Simba akakabidhiwa kombe, medali na fedha milioni 15 kama zawadi.

Kwa mujibu wa waandaji wa mashindano hayo, Mashindano hayo yatakuwa ya muendelezo huku sifa pekee ya vilabu waalikwa vikiwa ni kuwa mabingwa wa ligi kuu kwa nchi wanayotoka. 

Kwa upande wa tuzo binafasi, wachezaji wa Simba watano waliibuka na tuzo hizo. Bernard Morrison alipata tuzo ya kuwa mfungaji bora baada ya kufunga mabao 2 dhidi ya Al Hilal, Larry Bwalya alipata tuzo ya mchezaji bora, Beno Kakolanya tuzo ya golikipa bora na Luis Miquissone, nyota wa mchezo.

Simba wametimiza lengo lao la kuanzisha Simba Super Cup?

Lengo lilikuwa na kuwapata wachezaji utimamu wa mwili kuelekea michezo ya makundi, kwa kiasi fulani hilo wamefanikiwa. Wachezaji wamepata michezo miwili yenye hadhi ya upinzani ambao Simba waliutaka. Hongera sana Simba.

Simba watashuka dimbani terehe 2 Febrauri kucheza na Dodoma Jiji na tarehe 7 Februari watakipiga na Azam ikiwa ni michezo yake ya viporo kabla ya kuwavaa AS Vita ugenini nchini DR Congo kwenye klabu bingwa Afrika.

Michezo miwili ya Al Hilal na TP Mazembe ni sehemu moja ya kupasha misuli kuelekea michezo ya makundi, lakini ukijumlisha michezo miwili mingine ya VPL inamaana Simba watakuwa kwenye nafasi kubwa zaidi ya kupata utimamu wa mwili na utayari wa kuwavaa AS Vita Februari 12, 2021.

Maandalizi sio utimamu wa mwili tu kama nyama, ila ni utimamu wa kiakili pia. Kupitia maandalizi ya Simba Super Cup na kufanikiwa kubeba kombe hilo basi akili za wachezaji wa Simba ziko shwari, zina amani, zina umoja, zina utulivu na zimesahau kukosa kombe la mapinduzi kwa Yanga.

Kuna faida nyingine nyingi kwa Simba kupitia Simba Super Cup, faida hizo ni kama zifuatazo: Simba wamempa fursa mwalimu kuona kikosi na kujua uwezo kiasi wa wachezaji wake, Simba haitokuwa na uwoga wa mechi endapo ikitokea wakakutana na Al Hilal au TP Mazembe kwenye hatua zinazofuata.

Simba imepata mazoezi mazuri kutoka kwa wapinzani wanaofafana aina ya uchezaji na wapinzani ambao wanaokwenye kundi A, Al Merick ikitoka nchi moja na Al Hilal wakati AS Vita ikiwa ni wapinzani halisi ya TP Mazembe nchini Congo DR.

Wachezaji wamepata eneo la kujenga uhusiano na kocha wao mpya kitu ambacho kitawasaidia sana kwenye dressing room, mfno mchezaji Bernard Morrison kufunga mabao mawili na kuwa mfungaji bora imempa utulivu wa akili na kurudisha umakini kwa kocha wake.

Hizo zikiwa baadhi kwenye eneo la kifundi na kitimu, pia Simba wamenufaika nje ya uwanja, Simba imejenga mahusiano mazuri ya kirafiki na vilavu vya Al Hilal na TP Mazembe, mahusiano hayo yatawaruhusu Simba kujifunza mengi mazuri kwenye kuendesha timu kisasa na kufikia malengo.

Ndoto kubwa ya Simba ni kutaka kutwaa kombe la klabu bingwa Afrika, na hatua wanazopitia zimeshapitiwa na TP Mazembe chini ya mmiliki wake Bilionea, Moise Katumbi, hivyo ni rahisi kubadilishana mawazo na mmiliki wa Simba Bilionea Mohamed Dewji 'MO'.

Simba imezidi kuteka vyombo vya habari kwengineko Afrika na Duniani baada ya kuvialika vilabu maarufu na vyenye ushawishi Afrika husuani TP Mazembe ambaye ni bingwa mara tano wa kombe la klabu bingwa Afrika.

Umaarufu huo pia ni mvuto zaidi kwa wachezaji na makocha kufikiria kucheza na kuifundisha Simba kwa siku za usoni. Umaarufu huo, unaongeza thamani ya Simba kibiashara Afrika na kimataifa zaidi.

Simba imepata mapato kupitia watu waliohudhuria uwanja wa Benjamin William Mkapa kushuhudia michezo hiyo na kuwasaidia kupunguza makali ya matumizi kwa kile kinachoaminika wametumia fedha nyingi kuandaa mashindano hayo.

Lengo mama lilikuwa ni kuwapata utimamu wachezaji kupitia hiyo michezo miwili, lakini pia zimejitokeza faida nyingine nyingi. Hongera sana kwa Wekundu wa Msimbazi Simba.

Maboresho yawepo kwenye maeneo gani?

Kwanza, idadi ya timu iongezeke, nadhani moja itatosha kwa maana timu ziwe nne. Mazoezi yazidi kwa wachezaji. Pili promo isiishie sana Tanzania, izidi kwenda kimataifa zaidi ili kujitangaza. Nadhani kwa sasa itakuwa ngumu kupata faida za fedha kupitia mapato ya getini lakini faida za nje ni nyingi.