Wednesday , 5th Nov , 2014

Familia moja jamii ya wafugaji Wilayani Handeni, Mkoani tanga imevamiwa, kuchomewa nyumba na kujeruhiwa kwa mapanga na watu wasiojulikana.

Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga ACP Frasser Kashai

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kilimila Ng'ombe kilichopo kata ya Chanika wilayani Handeni wamevamia familia moja ya jamii ya wafugaji iliyopo katika kijiji hicho kisha kuwakata kwa mapanga baadhi ya akina mama na kuchoma moto nyumba moja ya familia hiyo.

Mgogoro kati ya wakulima na wafugaji umekuwa ni wa muda mrefu pasipo kutafutiwa ufumbuzi wa kina.

Wakizungumza na EATV wakazi wa kijiji hicho wamesema tukio hilo limetokea majira ya saa 8 mchana ambapo baadhi ya watuhumiwa walikwenda na mafuta ya taa na petrol kwa lengo la kuteketeza kitongoji chao kisha kufanya uharibifu wa mali na kuwapiga baadhi ya watu waliokuwepo katika nyumba hizo pamoja na mifugo yao ambayo baadhi yake imepata ulemavu.

Wakati huo huo Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga ACP Frasser Kashai amewaagiza askari wake kuhakikisha kuwa wanawakamata wahalifu wa tukio hilo ambao baadhi yake inadaiwa kuwa wamekimbilia wilaya ya Kiteto iliyopo mkoani Manyara hivyo amewataka wananchi kutoa taarifa za matukio ya uhalifu na jeshi litahakikisha linaficha siri zitakazo wezesha kukamatwa kwa watuhumiwa.

Katika hatua nyingine kamanda kashai amesema watu sita wanaosadikiwa kuwa majambazi wamevamia nyumba ya mvuvi Ally Faki katika eneo la kijiji cha Mwaboza kilichopo kata ya Moa jirani na mpakani mwa Kenya na Tanzania kisha kumpora fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 1.2 kisha kutoweka.