Wednesday , 7th Oct , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli amemuahidi rais wa Malawi Lazarus Chakwera kwamba Tanzania itaendelea kuboresha miondombinu yake ya usafiri ili kuimarisha zaidi ushirikiano wa kibiashara baina ya mataifa haya mawili.

Kushoto ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli, kulia ni Rais wa Malawi Dkt Lazarus Chakwera.

Rais Dk. Magufuli ametoa kauli hiyo leo akiwa na mgeni wake rais Chakwera Ikulu ya Dar es Salaam katika siku yake ya kwanza ya ziara yake nchini, ambapo amesema kwamba anataka nchi ya Malawi isijihisi kama isiyo na bahari yaani (land locked country).

Katika mazungumzo yao ya siku ya kwanza marais hao wamezungumzia masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya uchukuzi ili kurahisisha usafiri wa bidhaa kutoka na kuingia nchini Malawi.

Aidha Magufuli, amesema kuwa ziara ya siku tatu ya Rais wa Malawi Dkt Lazarus Chakwera, imeleta mafanikio na kufungua ukurasa mpya wa mashirikiano ya kibiashara, huku akiwataka wana Malawi wakija nchini wajisikie wako nyumbani.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli ameongeza kuwa urafiki wa nchi ya Malawi na Tanzania ni wa muda mrefu na kwamba wataendeleza ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo madini, kilimo, uvuvi pamoja na masuala ya ukusanyaji wa mapato.