Monday , 5th Oct , 2020

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefuta mafunzo ya ualimu wa shule ya msingi na awali kwa ngazi ya cheti, badala yake mafunzo yataanzia ngazi ya Stashahada (Diploma).

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt Avemaria Semakafu.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Avemaria Semakafu, amesema kuwa wizara imefanya maboresho ya mtaala wa ualimu wa awali na shule za msingi ambayo itatolewa kwa kipindi cha miaka mitatu na mafunzo ya cheti hayatotolewa tena.

“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefuta mafunzo ya ualimu wa shule ya msingi na awali kwa ngazi ya cheti, badala yake mafunzo yataanzia ngazi ya Stashahada (Diploma)“ amesema Semakafu.

Akizungumzia walimu walioko mashuleni tayari amesema “Walimu wenye vyeti waliopo makazini wasiwe na wasiwasi hakuna mtu atakayeondolewa kazini, haya ni maboresho tu na wataelekezwa namna ya kujiendeleza endapo wakihitaji kufanya hivyo”.

Kwa upande wake Mkurugenzi Taasisi ya Elimu, Dkt.Aneth Komba amesema kuwa walimu wa shule za msingi walikuwa wakimaliza stashahada na kusoma shahada walikuwa wanahamia shule za sekondari na kupelekea upungufu kwa walimu wa shule za msingi, hivyo maboresho ya mtaala yatasaidia kupata Maprofesa na Madaktari walimu wa shule za msingi na awali.