Thursday , 1st Oct , 2020

Mgombea urais wa Tanzania, kupitia Chama cha ADA TADEA, John Shibuda, amekosoa vikali mrengo wa siasa za majimbo, unaohubiriwa na chama cha siasa kimojawapo hapa nchini kwa kusema mpango huo utawagawa wananchi.

Mgombea urais kupitia Chama cha ADA TADEA, John Shibuda.

Kulingana na Shibuda aliyewahi kuwa Mbunge wa Maswa kwa miongo miwili mfululizo 2005-2015, akiingia Ikulu ya Chamwino atatupilia mbali fikra za siasa hizo za majimbo, akidai zikiruhusiwa zitaasisi ubaguzi wa kikanda na kikabila unaoweza kuleta mifarakano ya kugombania mikataba na rasiliamali.

“Kuna watu wanaonadi sera za majimbo, mimi sikubaliani kabisa na sera hizo kwani zikiruhusiwa zitawagawa Watanzania na kuleta ubaguzi wa kikanda na ukabila unaoweza kuleta mifarakano na kugombania rasilimali,” alisema Shibuda.

Mwanasiasa huyo aliyewahi kuhudumu ndani ya Chama Tawala (CCM) nafasi ya ubunge, kabla hajahamia upinzani mwaka 2010, amesema akiwa rais atalinda umoja wa kitaifa na uhuru wa kidemokrasia kwa vyama vyote vya siasa nchini.

Mgombea urais huyo aliyewahi kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) miongo miwili iliyopita kabla kuhamia ADA TADEA, amemsifu Rais Dk. John Magufuli, akidai kasimamia nidhamu kwa watumishi serikalini na kupambana na ufisadi.

John Shibuda, ambaye ni Mwenyekiti wa ADA TADEA, Mwenyekiti pia wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, aliyasema hayo alipokuwa akihutubia wananchi katika mkutano wake wa kampeni, uliofanyika eneo la Sangamwalugesha, Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu.

Shibuda anagombea urais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa mara yake ya kwanza, kati ya wagombe 15 wanaochuana na Rais John Joseph Pombe Magufuli, anayewania kuongoza Watanzania kwa muhula wa pili na wa mwisho, kulingana na takwa la Katiba ya nchi.