Thursday , 24th Sep , 2020

Kufuatia Tanzania kutangazwa na benki ya dunia kuwa nchi ya uchumi wa kati , wito umetolewa kutungwa sheria ambayo itatoa miongozo kwa viongozi watakaoingia madarakani kuendeleza sera za maendeleo ili kukuza mafanikio ya uchumi yaliyosimamiwa na viongozi wa utawala unaoacha madaraka.

Ushauri huo umetolewa na wadau wa sheria na uchambuzi wa siasa wakati wa mahojiano na EATV ambapo wamesisistiza uwepo wa sheria hiyo kuwa utasaidia kuendeleza sera chanya za ukuaji wa uchumi.

“Ukiangalia kila kiongozi  utakuta ameweka  mikakati ambayo ipo  katika kuhakikisha kuna kuwa na uwezo wa kushindana na kuboresha uchumi kutoka katika utegemezi wa sekta moja pekee.” Henry Mwinuka Wakili

Kwa upande wake Wakili na Mchambuzi wa siasa Dkt. Onesmo Kyauke, amesema nchi  zilizofanikiwa kufikia uchumi wa kati zimekuwa na mkakati wa uwekezaji katika sekta mseto ili kusaidia kuendelea kukuza sera zake na hivyo kupanda zaidi.

“Vipo vigezo vingine ambavyo vimewekwa katika dira ya maendeleo ikiwemo mikakati ya uboreshaji wa miundombinu,huduma mbalimbali ya kisekta.”

“Vyama vya siasa vituambie katika ilani zao namna ya utekelezaji,kukosa muongozo huo umeturudisha nyuma haswa katika elimu mfano sera ya UPE enzi za mwalimu Nyerere ambayo ilisaidia kwa zaidi ya asilimia 90,baada ya hapo hali ilibadilika kutokana tu na sera za serikali zilizoteuliwa” alisema Dkt Onesmo Kyauke