Muuza machungwa akisubiri wateja sokoni baada ya kushusha kwenye gari kutoka mikoa inayozalisha bidhaa hiyo.
Eatv imefuatilia suala hili kujua changamoto hiyo kwa kuanzia kwa mkulima wa machungwa katika mkoa wa Tanga ili kufahamu zaidi kuhusu biashara hiyo kwa kuanzia ngazi ya wakulima na hapa mkulima Ally Mohamed anatoa ufafanuzi.
Kwa upande wao wafanyabiashara wa jumla katika soko la Tegeta Nyuki jijini humo wanasema suala la bei ya matunda hayo ambayo msimu wake unakaribia kuisha huanzia shambani ambapo lawama nyingi wamewatupia madalali ambao hutajwa kuongeza bei maradufu kabla ya kumfikia mlaji.
"Sio suala la kuisha msimu ila ukweli kumekuwa hakuna uwiano sawa katika biashara hii dalali akishafanya yake haangalii maslahi ya upande wa pili ambao ni wetu sisi na hadi bidhaa kumfikia mteja wa chini kabisa" amesema Omar Mkama
Je ni kweli madalali ndio sababu kuu ya kupanda bei ya machungwa? ambayo kwa sasa huuzwa kati ya shilingi 90 hadi 130 kwa bei ya jumla ikilinganishwa na 30 hadi 80 kwa bei ya awali Rajabu Naondo anafafanua huku akitoa ushauri.
"Hapa kipindi cha nyuma tulikuwa tunapakua magari matatu hadi manne lakini sasa hivi yanachukua hadi siku nne kumaliza magari hayo,nadhani kuwepo na mkakati mbadala haswa baada ya changamoto ya Corona kwa nchi jirani nashauri wamiliki wa viwanda kuona fursa hii itakayomsaidia pia mkulima kukua kiuchumi"
Joseph Sembo ni muuza machungwa kwa bei ya rejareja katika eneo la Bamaga jijini Dar es salaam anasema amefanya biashara hiyo kwa miaka zaidi ya sita kwa sasa anasema awali alikuwa akiuza na kumaliza mzigo kwa siku ila kwa sasa kutokana na bei analazimika kuuza mzigo huo kwa siku tatu.
"Hii biashara ndio maisha yangu ndio familia yangu inategemea kwa kila kitu ila kwa sasa hali imekuwa mbaya sana, nshindwa kupata matapo kama ya awali lakini natumia nguvu nyingi kumshawishi mteja kutokana na bei iliyopo"
Matunda ya machungwa mengi hulimwa mkoani Tanga katika eneo la Handeni, Muheza na katika maeneo machache ya wilaya ya Mkinga na Pangani bado wakulima wanatoa kilio chao kwa wasimamizi na watafiti kuhusu upatikanaji wa mbegu bora pamoja masoko ya uhakika ili kukuza uchumi binafsi na taifa kwa ujumla.