Wednesday , 22nd Jul , 2020

Uongozi wa klabu ya soka ya Azam Fc umesema haina mpango wa kuziwania saini ya nyota wa klabu ya Yanga, Benard Morrison na Papii Kabamba Tshishimbi katika dirisha la usajili lijalo.

Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa Azam FC, Zacharia Thabit (Pichani) akiwa katika studio za East Africa Radio akizungumzia mikakati yao kuelekea msimu ujao.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa idara ya Habari na Mawasiliano wa Azam Fc, Zacharia Thabit ambaye amesema licha ya kuja na mkakati kabambe wenye lengo la kufanya usajili wa aina yake wenye msemo wa ''Kumega), lakini hawajadhamiria kuchukua wachezaji wasioendana na falsafa zao.

Zaka Zakazi amesema mchezaji kama Morrison anakuzwa sana kutokana na klabu anayoichezea ambayo ina washabiki wengi, lakini hana kiwango cha kutisha kiasi cha wao kutumia pesa nyingi kuvunja mkataba, sawa na Tshishimbi ambaye anaamini wachezaji wa aina yake wapo katika klabu yao ya Azam.

Ameongeza kuwa kauli yake ya kuwa watu wachukue tahadhari haikua ina maanisha ni vilabu vya Simba na Yanga, bali ni mataifa ya jirani yenye wachezaji wa viwango vya juu kuliko hapa nchini, na anaamini watarejesha heshima ya ushindani wa klabu yao katika ligi kuu msimu ujao.

Mashabiki wa soka nchini walianza kufuatilia kuwa ni timu ipi itabomolewa na Azam ambayo imempa nguvu kocha wake Aristica Cioba kusajili wachezaji hata 15 , kutokana na mahitaji yake na wao wapo tayari kutumia kiasi cha fedha kufanikisha mkakati huo.