Thursday , 16th Jul , 2020

Wakati Tanzania ikielekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, viongozi wa Dini mbalimbali wamewaonya viongozi wa siasa kutotumia Dini kugawanya watu katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu.

Viongozi wa Dini.

Hayo yameelezwa na Askofu Nelson Kisare, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu, Kanisa la Mennonite Tanzania na Mjumbe wa CCT, pamoja na Sheikh Mohammed Khamis ambaye ni Naibu Katibu Mkuu BAKWATA, wakati wa uzinduzi wa mwongozo wa uanzishaji na uendeshaji wa Kamati za mahusiano na ushirikiano wa viongozi wa Dini mbalimbali nchini, ambao unaonesha nafasi ya viongozi wa dini katika kudumisha amani na haki za jamii.

"Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba, viongozi tuwe mstari wa mbele kukemea matendo maovu ikiwemo watu wanaotumia miamvuli ya dini kuvuruga amani na kuleta migogoro katika jamii”, amesema Askofu Kisare.

Kwa Upande wake, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, amewataka wanawake kuwania nafasi za uongozi na wasibaki kuwa wapiga kura pekee.

"Akina Mama wahamasishwe na viongozi wa Dini kujitokeza kuwania nafasi za uongozi, maana wao ndiyo walezi wa familia wanaelewa nchi inahitaji kitu gani na kwa wakati gani", amesema Padre Kitima.