Thursday , 9th Jul , 2020

Uongozi wa klabu ya Polisi Tanzania ya mkoani Kilimanjaro, imeyapokea kwa shingo upande mabadiliko ya ratiba ya mchezo wao wa ligi kuu ya Tanzania bara baina yao dhidi ya Mbeya City uliotakiwa uchezwe jana katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Kikosi cha klabu ya Polisi Tanzania(Pichani).

Akizungumza na kipindi cha michezo cha Kipenga, East Africa Radio, Afisa Habari wa klabu hiyo Frank Lukwaro amesema kuwa kusogezwa kwa mchezo huo wa siku mbili utaigharimu timu yao kiuchumi, kwa kuwa hawakutegemea kukaa kwa siku mbili zaidi katika mkoa wa Mbeya.

Lukwaro ameongeza kwamba, wameishi katika jiji la Mbeya kwa siku 11 hadi siku ya jana, na gharama za kuifanya timu ikapata chakula na malazi, ni wazi kwamba bajeti yao inaongezeka.

Pamoja na hayo Afisa Habari huyo amesema sababu za kuipa muda Mbeya City muda wa kujiandaa na mchezo wao kutokana na wao kucheza mchezo wao siku ya juma nne ina mashiko,lakini upande wao haitowasaidia kwa chochote.

Polisi Tanzania imeshinda mechi moja kati ya tano za mwisho, ikitoka sare michezo mitatu na kufungwa mmoja, na sasa ipo katika nafasi ya sita kwa alama zao 48.

Kwa upande wa wapinzani wao katika mchezo wa siku ya Ijumaa, Mbeya City haijawa na matokeo mazuri msimu huu, kwa sasa wapo katika nafasi ya 18 wakiwa na alama 36 ingawa wameshinda michezo yao miwili ya mwisho waliyoteremka dimbani.