Friday , 1st May , 2020

Balozi Dkt Augustine Mahiga alizaliwa Agosti 28, 1945, Kijiji cha Tosamaganga mkoani Iringa, alisoma elimu yake ya Msingi na Sekondari hapa nchini na baadaye mwaka 1968, alijiunga na Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, DSM na kuhitimu Shahada ya Sanaa akibobea kwenye Elimu mwaka 1971.

Marehemu Balozi Dkt Augustine Mahiga, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Baadaye alipata ufadhili wa masomo yake nchini Canada, katika Chuo Kikuu cha Toronto na kuhitimu Shahada ya Sanaa na baadaye aliendelea na masomo katika chuo hicho hicho akijikita katika uhusiano wa Kimataifa na kuhitimu mwaka 1975 .

Mwaka 1980 hadi 1983, Balozi Dkt Mahiga alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, baadaye pia aliteuliwa kuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Kimataifa akifanya kazi Geneva - Uswisi, ambapo baadaye mwaka 1992 na 1994 aliteuliwa kuwa kiongozi mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR).

Balozi Dkt Mahiga ni Mwanadiplomasia wa Tanzania na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Tanzania kutoka 2015-2019 na hapo awali aliwahi kuwa Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwa Umoja wa Mataifa, kutoka 2003 hadi 2010 na kama Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa (UN) na Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Umoja wa Mataifa kutoka Somalia 2010 hadi 2013.

Mnamo Machi 03, 2019, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, alimteua Balozi Dkt Augustine Mahiga kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, akichukua nafasi ya Profesa Palamagamba Kabudi, na aliapishwa Machi 4, 2019

Balozi Dkt Augustine Mahiga ameaga Dunia mapema leo Mei 1, 2020, Jijini Dodoma, baada ya kuugua ghafla.

Mungu ailaze roho ya Marehemu Balozi Dkt Augustine Mahiga, mahala pema peponi. Amina.