Friday , 1st May , 2020

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Profesa Sifuni Mchome, amepongeza utendaji kazi wa aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Augustine Mahiga, na kusema kuwa alikuwa ni mnyenyekevu kwa kila mtu na alikuwa anatoa mawazo mbalimbali licha ya kwamba hakuwa ni Mwanasheria.

Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt Augustine Mahiga na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Sifuni Mchome.

Profesa Mchome ameyabainisha hayo wakati akizungumza na Supa Breakfast ya East Afrika Radio, na kusema kuwa kifo cha Dkt Mahiga kimekuwa ni pigo kubwa kwa wafanyakazi na Wizara kiujumla.

"Waziri wetu huyu Dkt Mahiga, ni mtu ambaye alikuwa ni mnyenyekevu kwa kila mtu na alikuwa anafanya kazi kwa ukaribu na ni msikivu, alikuwa anatoa mawazo mbalimbali katika maeneo mengi, pamoja na kwamba hakuwa Mwanasheria lakini ulikuwa unaona kabisa anafikiri kama watu walioko kwenye hiyo fani ya Sheria" amesema Profesa Mchome.

Kifo cha Balozi Dkt Augustine Mahiga, ambaye alikuwa ni Waziri wa Katiba na Sheria kimetokea Alfajiri ya leo ya Mei 1, 2020, Jijini Dodoma, baada ya kuugua ghafla.