
Mzee Michael Mwita, Mstaafu wa JWTZ
Mzee Mwita ameyabainisha hayo wakati akizungumza na EATV, ambapo yeye ni mkazi wa Sokoni One, mkoani Arusha, na kusema amefikia hatua ya kuomba msaada huo kwa Watanzania na Serikali kiujumla, kutokana na hali yake kuwa mbaya zaidi kwani hajiwezi hata kutembea na kula kwake ni kwa shida.
"Mimi hapa ninapokaa nyumba yangu iliungua kutoka hapo hali yangu mpaka leo ni mbaya sana, sijiwezi kutembea na tangu hapo sina mtu wa kunipa chakula, ninakula kwa shida na sina kazi yoyote ninayoifanya mimi ninaomba msaada Serikalini" amesema Mzee Mwita.
Mzee Mwita ana umri wa miaka 96, ni mzaliwa wa Musoma Mkoani Mara, na ni mtoto wa kwanza kati ya watoto watatu, ambapo ndugu zake hao walikwishafariki na akabaki mwenyewe.
Lakini pia ana mke mmoja ambaye ni Bi Elizabeth Kimolo na wote walijaliwa kupata watoto nane, na kwa madai yake watoto nao hawana msaada wowote kulingana na hali zao za maisha kuwa ni ngumu.