Monday , 27th Apr , 2020

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa amesema kuwa marehemu Evod Mmandi, ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya Moyo na Sukari ambapo hali yake ilibadilika siku ya ijumaa na kulazwa kwenye Hospitali ya Ligula.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa.

Hayo ameyabainisha leo Aprili 27, 2020, wakati akitoa taarifa ya mazishi yake, ambapo amesema kuwa familia yake imeridhia kuwa mazishi hayo yatasimamiwa na Serikali na kufanyika mkoani humo na kuhudhuriwa na watu si zaidi ya 10.

"Tuko kwenye kipindi kigumu sana ambacho ni cha ugonjwa wa Corona na makatazo mbalimbali ya Serikali ya kuzuia mikusanyiko, kutokana na utaratibu huo, niishukuru familia ya marehemu, tumekubaliana sisi Serikali ndiyo tutakaosimamia mazishi yake, hakutakiwa na kusafirisha mwili, mazishi yatafanyika hapa Mtwara na hayatahudhuriwa na watu zaidi ya 10" amesema RC Byakanwa.

Marehemu Evod Mmandi, amefariki Dunia usiku wa kuamkia leo, ambapo alianza kuhudumu nafasi yake ya Ukuu wa Wilaya mwaka 2016, baada ya kuteuliwa na Rais John Pombe Magufuli.