Tuesday , 14th Apr , 2020

Wakati  jitihaha za kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa watoto zikiendelea, hali ni tofauti mkoani Iringa baada ya mtoto wa mwaka 1 mkazi wa eneo la Itunundu Pawaga, Wilayani Iringa kunusurika kifo kutokana na kupigwa na baba wa kambo.

Baadhi ya wasamaria wema waliojitokeza kuona mgonjwa katika hospitali ya Wilaya ya Iringa

Imeelezwa kuwa mtoto huyo alipigwa na baba yake wa kambo pamoja na kunyimwa chakula, ambapo baadaye aliokolewa na wasamalia wema.

Frola Kasuga, mama mzazi wa mtoto huyo ameleza kuwa baba wa kambo wa mtoto amekuwa akimfanyia visa ikiwemo kumfungia ndani ya nyumba huku akiwanyima chakula akidai kuwa ni kwa sababu mtoto si wake.

Baadhi ya wasamaria wema waliofika katika Hospitali teule ya Ipamba Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wamelaani vitendo hivyo, ambapo pamoja na kutoa pole wametoa msaada wao kwa mama na mtoto huyo.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Leah Mongwila amesema kuwa ukatili dhidi ya watoto ni suala lililokuwepo katika wilaya hiyo kwa muda mrefu na katika kipindi cha wiki moja, watoto takribani wanne wameripotiwa kwa kufanyiwa ukatili.

Kufuatia tukio hilo, mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi, ambapo atafikishwa mahakamani kwa uchunguzi zaidi huku wito ukitolewa kwa jamii kutoa taarifa za vitendo hivyo katika maeneo husika pindi zinapotokea.