Friday , 28th Feb , 2020

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi, imewachukulia hatua mbalimbali Makatibu Wakuu wawili Wastaafu, Abdulrahman Kinana na Mzee Yusuph Makamba, ikiwemo kutoa msamaha kwa Mzee Makamba pamoja na adhabu kwa Mzee Kinana.

Makatibu Wakuu wastaafu wa CCM, Yusuph Makamba na Abdulrahman Kinana.

Taarifa hiyo imetolewa leo Februari 28, 2020, na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Hamphrey Polepole, mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho kilichoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli, na kwamba Mzee Makamba tangu asomewe mashtaka yake amekuwa mnyenyekevu na mtii kwa mamlaka ya chama.

"Kamati Kuu imepokea maelezo ya Abdulrahman Kinana, na imeadhimia apewe adhabu ya karipio kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili, atakuwa hali ya matazamio kwa muda usiopungua miezi 18 kuanzia leo, ili ajirekebishe, na hatokuwa na haki ya kugombea nafasi yoyote katika chama" amesema Polepole.

Makatibu Wakuu hao wastaafu, miezi kadhaa nyuma waliibua mijadala mitandaoni baada ya sauti zao kuvuja, wakizungumzia uwepo wa mpasuko ndani ya CCM.