
Baadhi ya viongozi wa Sekretarieti ya Yanga na baadhi ya wachezaji wake
Bila kupepesa jicho, kitu pekee kinachowapa furaha 'Wekundu wa Msimbazi' hivi sasa ni mabadiliko ya mfumo wa kiuendeshaji uliobadilisha mambo kuwa juu chini ambapo sasa Simba ile iliyokuwa iki'balaswa' na Yanga kwenye kila nyanja ikiwemo kukosa ubingwa wa ligi mara tatu mfululizo, inacheka na kula supu ya pweza kila siku.
Wengi mtakumbuka ile misimu ambayo Yanga imechukua ubingwa mara tatu mfululizo kuanzia 2014/15 hadi 2016/17 ambapo 'Wanajangwani' hao walikuwa chini ya kivuli cha tajiri Yusuf Manji ambaye alikuwa akimwaga pesa kadri alivyojisikia ndani ya klabu hiyo, huku Simba wakilia njaa kali iliyopelekea kuporomoka kwa kiwango ndani ya wanja na kuwakosa wachezaji mastaa, hali iliyopelekea kutumia vijana kama Ibrahim Ajib, Said Ndemla, Mohamed Hussein, Haruna Chanongo na Miraji Adamu.
Baada ya kubadili mfumo wa uendeshaji na kumpata mwekezaji ambaye pia ana mahaba na klabu hiyo, Mohamed Dewji, sasa mambo yamebadilika na tunavyozungumza hivi sasa Simba ina uwanja wake wa mazoezi, ina kikosi ghali zaidi Tanzania na inajivunia mafanikio ya kufika hatua ya robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika huku ikiwa na ndoto ya kushinda ubingwa huo katika miaka ya karibuni.
Kutokana na mafanikio hayo, Yanga imeanza kuzungumzia namna ambavyo itaingia katika mabadiliko hayo ambapo kauli ya hivi karibuni ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dr. Mshindo Msolla imedhihirisha kiu ya mabingwa hao wa kihistoria kuondokana na hali mbaya ya kiuchumi iliyo nayo hivi sasa.
"Kamati ya kubadili mfumo wa uwekezaji wa klabu bado ipo na mimi nimefanya nao kikao, wananiambia kuwa watajitahidi ifikapo Mei-Juni 2020 tutaondoka katika utaratibu huu na twende katika mfumo wa uwekezaji", alisema Dr. Msolla katika mkutano wake na wanahabari.
Kwa maana hiyo, tutegemee kuona ushindani wenye tija endapo Yanga watafanikiwa kuingia katika uwekezaji na kuzidi kuifanya ligi ya Tanzania kuwa yenye ushindani na yenye mapato makubwa pamoja na kutoa ushindani katika michuano ya vilabu barani Afrika. Ni wazi kuwa wana lao kubwa moyoni na yanayoendelea katika klabu ya Simba, na kwamba ujio wao utakuwa wa kishindo ili kuonesha kuwa na wao si wanyonge kama wanavyofikiriwa lakini yote ni kwa ustawi wa mpira wa Tanzania.