Saturday , 26th Oct , 2019

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo, ameagiza wataalamu wa mitaala ya elimu hapa nchini kukaa na kutazama miongozo ya elimu iliyopo, kwani imewekwa kwa roho mbaya na inamnyima mwanafunzi uhuru wa kuchagua kusoma fani anayoipenda.

Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo

Kauli hiyo ameitoa leo Oktoba 26, 2019 wakati wa utoaji wa tuzo za Elimu kwa Wanafunzi wa Darasa la Saba waliofanya vizuri kwa mwaka 2019, ambapo ameagiza miongozo hiyo kuwekwa vizuri, kwani iliyopo sasa inaua vipaji vya watoto wengi bila wao kujua.

"Sisi kama Serikali tuache utaratibu wa kuua vipaji vya watu maana kuna miongozo inawekwa kuua vipaji vya watu, wataalamu muangalie miongozo mingine imewekwa kwa roho mbaya, mtoto aliyesoma CBG leo hii tunatangaza nafasi za ajira tunakosa mtu wa mionzi", amesema Waziri Jafo

"Mtu akisoma PCM ni lazima akawe injinia?, PCM hawezi kuwa Mfamasia?, inawezekana hata wazazi hawafahamu hii miongozo ina roho mbaya, watu wanapanga wamejifungia tu ndani kwa vile wao na familia zao maisha yameisha, hawajui hata watanzania wengine wanaishije", ameongeza.

Aidha Waziri Jafo amemuagiza Katibu Mkuu TAMISEMI, kuhakikisha wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani yao ya darasa la saba wanapewa nafasi ya kuchagua shule za Serikali wanazopenda kwenda kusoma na si kuwapangia shule zingine tofauti na watakazozichagua.