Wednesday , 18th Sep , 2019

Wakili wa kujitegemea na aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Fatma Karume, ameonesha kushangazwa na kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, iliyoeleza kinachomuweka madarakani ni njaa tu na kusema kwamba, kiongozi huyo inaonesha ni kwa namna gani hawezi

Fatma Karume

Akizungumza leo Septemba 18, 2019 na EATV&EA Radio Digital, Fatma Karume amesema kuwa kwa kiongozi yeyote aliyepewa jukumu la kuhudumia wananchi, hakupaswa kutanguliza maslahi yake binafsi.

''Mimi nilikuwa nategemea kwamba, mtu anaingia katika utumishi wa Umma kwa ajili ya huduma kwa wananchi, sasa ukikubali kufanya kazi kama RC na umepewa kazi hiyo na Rais ni kwamba uko  tayari kuwahudumia wananchi, lakini kwa maneno aliyoyasema Makonda yeye yupo pale kujihudumia mwenyewe na njaa zake'' amesema Fatma Karume.

Aidha Wakili huyo ameongeza kuwa,kutokana na kauli hiyo, Makonda ameudhihirisha Umma kwamba hauwezi kusimama peke yake.

''Tatizo ni kwamba yupo pale kujihudumia njaa zake kwa maana huyu mtu hawezi kusurvive bila Serikali na anaitegemea Serikali na nguvu za wananchi ili ale, siyo yeye anayetaka awahudumie Wananchi bali anataka Wananchi wamhudumie yeye kitu ambacho hakiwezekani'' amesema Wakili huyo.

Kauli ya njaa ya  Makonda imekuja ikiwa ni siku chache tangu Rais Magufuli, alipotembelea machinjio ya Vingunguti na kuonesha kutoridhishwa na ujenzi wa machinjio mapya, ambapo alimuagiza Mkuu wa Mkoa kuhakikisha anasimamia miradi ya mkoa wake na inatekelezeka kwa muda muafaka.